Watu wengine 40 wauawa kwa kukatwa mapanga Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61262-watu_wengine_40_wauawa_kwa_kukatwa_mapanga_kongo_dr
Watu wasiopungua 40 wameuawa katika shambulizi jingine la kutisha la wanamgambo wa ADF huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mpakani na Uganda.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 28, 2020 03:29 UTC
  • Watu wengine 40 wauawa kwa kukatwa mapanga Kongo DR

Watu wasiopungua 40 wameuawa katika shambulizi jingine la kutisha la wanamgambo wa ADF huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mpakani na Uganda.

Hayo yalisemwa jana Jumatano na Omar Kavota, afisa wa shirika la kutetea haki za binadamu la CEPADHO na kuongeza kuwa: Mauaji hayo ya umati yalifanywa na wapiganaji wa ADF walioshambulia kijiji cha Samboko, kilichoko umbali wa kilomita 100 kusini magharibi mwa jiji la Bunia, mkoani Ituri.

Amesema magaidi hao walitekeleza ukatili huo kwa kutumia mapanga na kwamba mbali na mauaji, wameiba pia vitu vya thamani vya wakazi wa kijiji hicho.

Mauaji hayo ya halaiki yameripotiwa siku moja baada ya wamgambo hao wa ADF kushambulia kijiji cha Makutano mkoani Ituru, karibu na Bunia, na kuua raia 17.

Kwa mujibu wa kituo cha utafiti cha Kivu Security Tracker (KST), watu zaidi ya 400 wameuawa katika mashambulizi ya wanagambo wa ADF tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.

ISIS imekuwa ikijinasibisha na na genge la ADF

Mamia ya Wakongomani wameuawa katika mashambulizi ya wanamgambo wa ADF ambao asili yao ni Uganda hususan katika maeneo ya mashariki mwa nchi, tokeo mwaka 2014. 

Licha ya kundi hilo kutangaza kuwa na mfungamano na genge la kigaidi la ISIS, lakini wadadisi wa mambo wanasema hakuna ushahidi wowote wa kuyapa nguvu madai hayo.