May 31, 2020 11:38 UTC
  • 7 wauawa katika mripuko wa bomu karibu na Mogadishu, Somalia

Kwa akali watu saba wamepoteza maisha baada ya basi dogo lililokuwa limewabeba kukanyaga bomu la kutegwa ardhini kando ya barabara moja katika kijiji cha Hawa Abdi viungani mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Mashuhuda wanasema basi hilo dogo lilikuwa limebeba abiria waliokuwa wanaelekea Mogadishu kwa ajili ya shughuli za mazishi wakitokea katika mji wa Afgoye ulioko umbali wa kilomita 30 kusini magharibi mwa mji huo mkuu wakati wa mripuko huo wa mapema leo Jumapili.

Farah Hassan, afisa wa polisi karibu na eneo la tukio ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "hadi kufikia sasa tunafahamu kuwa mripuko huo umeua watu saba na kujeruhi wengine kadhaa, lakini yumkini idadi hiyo ikaongezeka."

Hakuna kundi lolote la kigaidi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo la bomu kufikia sasa.

Wanachama wa genge la kigaidi la al-Shabaab

Hata hivyo kundi la kigaidi a kitakfiri la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaidah limehusika na utegaji mabomu na mashambulizi mengi ndani ya Somalia na katika nchi jirani tokea mwaka 2007.

Haya yanajiri siku chache baada ya genge hilo la ukufurishaji kuua wanajeshi 14 wa Somalia katika mashambulizi mawili ya bomu katika eneo la Juba ya Kati (Mei 26) na Lower Shebelle (Mei 28).

Tags