Askari wa Uganda na Sudan Kusini wafyatuliana risasi, 4 wauawa
(last modified Wed, 03 Jun 2020 03:54:46 GMT )
Jun 03, 2020 03:54 UTC
  • Askari wa Uganda na Sudan Kusini wafyatuliana risasi, 4 wauawa

Kwa akali wanajeshi wanne wa Sudan Kusini wameuawa katika makabiliano ya risasi na wenzao wa Uganda mpakani mwa nchi mbili hizo jirani.

Hayo yalisemwa jana Jumanne na Lul Ruia Koang, msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Sudan Kusini (SSPDF) na kuongeza kuwa, makabiliano hayo ya risasi kati ya vikosi vya nchi hiyo na Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF) yalifanyika katika eneo la mpakani linalozozaniwa na pande mbili huko kusini mwa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Amesema, "askari wa UPDF walianza kuwafyatulia risasi wanajeshi wetu katika eneo la Buya, na kuua wanne papo hapo na kujeruhi mwingine mmoja."

Msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Sudan Kusini amesema askari wa nchi hiyo walikuwa wanashika doria ili kukabiliana na wanaotaka kujipenyeza nchini humo kinyume cha sheria kabla ya kuanza makabiliano hayo siku ya Jumapili.

Askari wa Sudan Kusini

Ameongeza kuwa, kwa sasa hali ya utulivu imerejea katika eneo hilo la mpakani baada ya serikali za nchi mbili hizo kuafikiana juu ya kufanyika uchunguzi wa tukio hilo la umwagaji damu.

Eneo hilo tata la mpakani linazozaniwa na jamii za kaunti ya Kajo-Keji jimbo la Central Equatoria la Sudan Kusini na majirani zao wa wilaya ya Yumbe ya Uganda.