Rais Kagame ataka kuondolewa vikwazo Zimbabwe na Sudan
Rais Paul Kagame wa Rwanda ametoa mwito wa kuondolewa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Zimbabwe na Sudan ili kuzisaidia nchi hizo katika vita dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.
Rais Kagame alitoa mwito huo jana Jumatano katika mkutano wa kwanza usio wa kawaida wa Jumuiya ya Mataifa ya Afrika, Caribbean na Pacific (OACPS) uliofanyika kwa njia ya video, chini ya uenyekiti wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Kagame amesema, "athari za Covid-19 zitaendelea kuwepo kwa muda mrefu hata baada ya kuvishinda virusi, na barabara ya kurejea katika hali ya kawaida itakuwa ndefu mno." Rais wa Rwanda amesema kwa msingi huo, kuna haja ya kuangaliwa upya suala la vikwazo dhidi ya Zimbabwe na Sudan ili kupiga jeki jitihada za nchi mbili hizo za Kiafrika za kupambana na mgogoro huo wa kiafya.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Mei, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe alizishambulia vikali nchi za Magharibi kwa kuendelea kuingilia masuala ya ndani ya mataifa ya Afrika na kueleza bayana kuwa, "Afrika imepinga na kulaani vikwazo dhidi ya Zimbabwe na Sudan, na kuwataka waliochukua hatua hizo haramu na za kihaini kuviondoa vikwazo mara moja bila masharti yoyote."
Kabla ya hapo pia, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye pia ni mwenyekiti wa hivi sasa wa Umoja wa Afrika (AU) alitaka kuondoloewa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi mbili hizo za Kiafrika hususan wakati huu wa mapambano dhidi ya janga la corona.
Itakumbukwa kuwa Marekani iliiwekea vikwazo Sudan kwa madai kuwa inaunga mkono ugaidi, madai ambayo yamekanushwa na serikali ya Khartoum. Aidha Marekani hivi karibuni ilirefusha vikwazo dhidi ya Zimbabwe vilivyokuwa vimewekwa wakati wa urais wa Barack Obama kwa madai ya kuweko ukandamizaji wa kisiasa nchini humo.