Wanamgambo wa CODECO waua watu 16 Kongo DR
Watu wasiopungua 16 wameuawa katika shambulizi jingine la kutisha la wanamgambo wa CODECO huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Henry Juga Trilo, afisa wa utawala katika mkoa wa Ituri amesema wanamgambo hao wa kabila la Walendu walivamia kijiji cha Moussa ambacho aghalabu ya wakazi wake ni wa kabila la Hema katika mkoa huo mapema jana na kutekeleza ukatili huo.
Afisa huyo wa serikali amesema waliouawa katika hujuma hiyo ya kikatili ni wanawake sita, wasichana sita na wanaume wanne mbali na mbuzi kadhaa kuibiwa na wanamgambo hao waliobeba silaha.
Msemaji wa Jeshi la DRC na duru za Umoja wa Mataifa zimethibitisha habari ya kujiri shambulizi hilo la umwagaji damu katika kijiji cha Moussa, yapata kilomita 60 kaskazini mashariki mwa jiji la Bunia mkoani Ituri, katika mpaka wa Kongo DR na Uganda.
Haya yanajiri katika hali ambayo, wiki iliyopita Umoja wa Mataifa ulitahadharisha kuwa, kuna uwezekano kumejiri uhalifu wa kivita huko Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya mamia ya watu kuuawa na makundi ya watu wenye silaha.
UN imesema katika kipindi cha miezi sita iliyopita, watu wasiopungua 296 wameuawa, 151 kueruhiwa na wengine 38 kubakwa, wakiwamo wanawake na watoto; na kwamba vitendo hivyo vya kikatili vilitekelezwa na waasi kutoka kabila la Walendu kati ya mwezi Novemba mwaka uliopita na mwezi Aprili mwaka huu.