Umoja wa Mataifa wapatwa na wasiwasi kufuatia kugunduliwa makaburi ya umati Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61555-umoja_wa_mataifa_wapatwa_na_wasiwasi_kufuatia_kugunduliwa_makaburi_ya_umati_libya
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini libya umeingiwa na wasiwasi mkubwa baada ya kugunduliwa makaburi ya umati magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2020 03:07 UTC
  • Umoja wa Mataifa wapatwa na wasiwasi kufuatia kugunduliwa makaburi ya umati Libya

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini libya umeingiwa na wasiwasi mkubwa baada ya kugunduliwa makaburi ya umati magharibi mwa nchi hiyo.

Jana Alkhamisi ujumbe huo ulitoa taarifa ukielezea wasiwasi mkubwa ulionao kuhusiana na ripoti za kutisha na kushtua kuhusu kugunduliwa kwa uchache makaburi manane ya umati ambapo mengi yapo katika mji wa Tarhuna na kutaka uchunguzi ufanyike mara moja kubaini chanzo cha mauji hayo ya umati na yanayokiuka sheria dhidi ya raia wasio na hatia.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umekaribisha uamuzi wa Muhammad Abdul Wahed Lamloom, Waziri wa Sheria wa Libya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, wa kubuni tume ya uchunguzi kuhusu suala hilo.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya jana Alkhamisi ilitangaza habari ya kugundulika kaburi moja lililokuwa na miili mitatu katika makao ya idara kuu ya usalama katikati mwa mji wa Tarhuna. Makaburi mengine manne tayari yalikuwa yamegunduliwa katika mji huo siku kadhaa zilizopita.

Mapigano ya ndani Libya

Kundi linalojiita Jeshi la Kitaifa la Libya linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar ambalo linaungwa mkono kwa miaka mingi sasa na Saudia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi, linadhibiti eneo la mashariki mwa Libya. Tokea mwezi Aprili mwaka uliopita kundi hilo limekuwa likifanya mashambulizi makali kuelekea magharibi mwa nchi kwa lengo la kuuteka mji mkuu, Tripoli, ambao unadhibitiwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Katika siku za karibuni jeshi la serikali limefanikiwa kuukomboa mji wa Tarhuna kutoka mikononi mwa wapiganaji wa Haftar.