Rais mteule wa Burundi kuapishwa Alkhamisi
Rais mteule wa Burundi, Evariste Ndayishimiye aliyeshinda uchaguzi mkuu wa hivi karibuni anatazamiwa kuapishwa Alkhamisi hii Juni 18 kuwa rais wa nchi hiyo kufuatia kifo cha ghafla cha Rais Pierre Nkurunziza.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Burundi jana Jumatatu ilituma mialiko kwa mabalozi na wanadiplomasia wa nchi za kigeni nchini humo, ikiwaomba wahudhurie hafla ya kuapishwa kwa rais huyo mteule.
Uamuzi wa kuapishwa mapema rais huyo mteule ulipasishwa na Mahakama ya Katiba ya Burundi. Alkhamisi iliyopita, Baraza la Mawaziri la nchi hiyo lilifikia uamuzi wa kuikabidhidi mahakama hiyo jukumu hilo, baada ya taifa hilo kushuhudia ombwe la uongozi kufuatia kifo cha Nkurunziza.
Kwa mujibu wa Katiba ya Burundi, Spika wa Bunge ndiye aliyepaswa kushika madaraka ya nchi hadi wakati wa kuapishwa rasmi rais mteule. Awali Ndaiyishimiye alitazamiwa kula kiapo hicho cha kulitumikia taifa mwezi Agosti mwaka huu.
Katika uchaguzi uliofanyika Mei 20 mwaka huu, Nkurunziza hakugombea na mgombea wa chama tawala CNDD-FDD, Jenerali Mstaafu Evariste Ndayishimiye ndiye aliyeibuka mshindi.
Rais Nkurunziza ambaye ameiongoza Burundi kwa miaka 15 alifariki dunia kwa kile ambacho serikali ilisema ni maradhi ya moyo mnamo tarehe 9 Juni mwaka huu wa 2020.