Ndayishimiye aapishwa kuwa rais mpya wa Burundi, aahidi kuliunganisha taifa+SAUTI
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61684-ndayishimiye_aapishwa_kuwa_rais_mpya_wa_burundi_aahidi_kuliunganisha_taifa_sauti
Evariste Ndayishimiye aliyeshinda uchaguzi mkuu wa hivi karibuni nchini Burundi ameapishwa leo Alkhamisi kuwa rais mpya wa nchi hiyo, kufuatia kifo cha ghafla cha Rais Pierre Nkurunziza.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Jun 18, 2020 13:25 UTC
  • Ndayishimiye aapishwa kuwa rais mpya wa Burundi, aahidi kuliunganisha taifa+SAUTI

Evariste Ndayishimiye aliyeshinda uchaguzi mkuu wa hivi karibuni nchini Burundi ameapishwa leo Alkhamisi kuwa rais mpya wa nchi hiyo, kufuatia kifo cha ghafla cha Rais Pierre Nkurunziza.

Hafla ya kuapishwa jenerali huyo mstaafu wa jeshi imefanyika katika mji mkuu wa kisiasa wa Gitega, ambapo ameahidi kuliunganisha taifa hilo ambalo limekatiwa misaada na wafadhili haswa wa nchi za Magharibi kwa madai ya kukanyaga haki za binadamu.

Rais Ndiyishimiye amesema, "sitofelisha mkataba wa amani, katiba na sheria zingine za nchi, nitadhumisha umoja miongoni mwa Warundi, amani na haki kwa wote, na pia nitakabiliana na idiolojia ya mauaji ya kimbari na ubaguzi."

Awali Ndaiyishimiye alitazamiwa kula kiapo hicho cha kulitumikia taifa mwezi Agosti mwaka huu. Uamuzi wa kuapishwa mapema rais huyo mteule ulipasishwa na Mahakama ya Katiba ya Burundi. Alkhamisi iliyopita, Baraza la Mawaziri la nchi hiyo lilifikia uamuzi wa kuikabidhidi mahakama hiyo jukumu hilo, baada ya taifa hilo kushuhudia ombwe la uongozi kufuatia kifo cha Nkurunziza. 

Hayati Pierre Nkurunziza

Kwa mujibu wa Katiba ya Burundi, Spika wa Bunge ndiye aliyepaswa kushika madaraka ya nchi hadi wakati wa kuapishwa rasmi rais mteule.

Katika uchaguzi uliofanyika Mei 20 mwaka huu, Nkurunziza hakugombea na mgombea wa chama tawala CNDD-FDD, Jenerali Mstaafu Evariste Ndayishimiye ndiye aliyeibuka mshindi kwa kupata asilimia 69 ya kura.

Rais Nkurunziza ambaye ameiongoza Burundi kwa miaka 15 alifariki dunia kwa kile ambacho serikali ilisema ni maradhi ya moyo mnamo tarehe 9 Juni mwaka huu wa 2020.

MAELEZO ZAIDI NA MWANDISHI WETU WA BUJUMBURA, HAMIDA ISSA....