Marekani yafuta visa za raia wa Burundi kufuatia mgogoro wa kidiplomasia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61787-marekani_yafuta_visa_za_raia_wa_burundi_kufuatia_mgogoro_wa_kidiplomasia
Marekani imeacha kutoa visa kwa raia wa Burundi wanaotaka kwenda nchini humo, hatua ambayo imeibua mgogoro wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 24, 2020 07:20 UTC
  • Marekani yafuta visa za raia wa Burundi kufuatia mgogoro wa kidiplomasia

Marekani imeacha kutoa visa kwa raia wa Burundi wanaotaka kwenda nchini humo, hatua ambayo imeibua mgogoro wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.

Marekani imechukua hatua hiyo kwa msingi wa madai kuwa serikali ya Burundi haijafanya vya kutosha ili kuwarudisha nyumbani raia wake wanaoendelea kuishi Marekani bila vibali.

Idara ya Uhamiaji Marekani inasema inawashikilia raia watano wa Burundi ambao wote wamepatikana na makosa ya jinai na kwamba kuna Warundi wengine 500 walioko nchini humo ambao pia wanatakiwa kutimuliwa lakini bado hawajakamatwa.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Ezéchiel Nibigira amepinga kauli hiyo ya Marekani na kusisitiza kuwa watu ambao Marekani inataka warudishwe nyumbani sio raia wa Burundi.

Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi akiapishwa

Hayo yanajiri baada ya Evariste Ndayishimiye kuapishwa Alhamisi iliyopita kuchukuwa nafasi ya Pierre Nkurunziza aliyefariki dunia Juni 8 mwaka huu.

Katika hotuba yake baada ya kula kiapo, Rais Ndayishimye alisema utawala wake utajikita katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi, kuboresha maridhiano, kuinua uchumi, kuwarejesha wakimbizi nyumbani na kuimarisha usalama kwa Warundi wote bila kuegemea upande wowote.