Zimbabwe kuwalipa wakulima wazungu fidia ya dola bilioni 3.5
Serikali ya Zimbabwe imeafiki kuwalipa wakulima wazungu fidia ya dola bilioni 3.5 kutokana na ardhi zao kuchukuliwa na serikali kwa ajili ya kuwapa wenyeji Waafrika.
Mapatano hayo yaliyotiwa saini Jumatano yanalenga kutatua mgogoro ulioibuliwa na sera ya rais wa zamani wa nchi hiyo Robert Mugabe ambaye alichukua udhibiti wa ardhi zilizokuwa zikikaliwa na wazungu na kuzirejesha kwa Waafrika wenyeji wa nchi hiyo.
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe akizungumza baada ya kutiwa saini mapatano hayo katika Ikulu mjini Harare amesema mapatano hayo ni ya kihistoria. Amesema kwa mujibu wa katiba ya Zimbabwe, wakulima hao wazungu watalipwa fidia kwa ajili ya miundomsingi ya mashamba na wala si kwa ajili ya ardhi.
Waziri wa Fedha wa Zimbabwe Mthuli Ncube amesema serikali iko mbioni kutafuta wafadhili wa kimataifa ili waweze kuisaidia serikali kulipa fidia hiyo.
Hatua ya rais wa zamani Mugabe ya kuchukua kwa nguvu ardhi ambazo zilikuwa zinamilikiwa na wazungu ambao walizipata wakati wa ukoloni ilikuwa chanzo cha kuzorota uhusiano baina yake na madola ya Magharibi. Mugabe, ambaye aliaondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi mwaka 2017 na kufariki mwaka jana, alizituhumu nchi za Magharibi kuwa ziliiwekea nchi yake vikwazo kama adhabu kwa kuwarejeshea wazalendo Waafrika ardhi ambazo zilikuwa zimeporwa na wazungu.