Idadi ya watu waliouawa kwenye ghasia nchini Sudan Kusini yaongezeka
Idadi ya vifo vya watu waliouawa katika machafuko ya jimbo la Warrap huko Sudan Kusini imeongezeka na kufikia 148 kufuatia mapigano yaliyojiri majuzi katika zoezi la kukusanya silaha zinazomilikiwa na wananchi.
Umoja wa Mataifa tayari umetuma askari jeshi wa kudumisha amani katika jimbo hilo.
Mapigano makali yalijiri kwa muda wa siku mbili kati ya raia wenye silaha na askari jeshi wa serikali ya Juba waliokuwa wakisimamia zoezi la upokonyaji silaha baada ya vijana kadhaa waliokuwa na silaha katika eneo la Tonj kuanza kupambana na askari usalama.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tonj Mashariki, Makuel Mabior Dhuol amesema kuwa idadi ya vifo imeongezeka kutokana na baadhi ya majeruhi kukosa matibabu ya haraka baada ya mapigano.
Mabior amesema kuwa hadi kufikia sasa miili ya watu 148 imekusanywa kutoka pande zote husika katika mapigano hayo. Miili 85 ni ya raia wa kawaida na 63 ni ya wanajeshi wa serikali.
Watu wengine 141 wamejeruhiwa katika mapigano hayo ya kukusanya silaha zinazomilikiwa na raia. Ujumbe wa Kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa Jumanne iliyopita uliwasili eneo la Tonj na umeweka kambi ya muda ili kusaidia juhudi za kuzuia machafuko zaidi katika eneo hilo.