Tahadhari kuhusu kutoweka utajiri wa Afrika
Rais wa zamani wa Afrika Kusini ameonya kuhusu bara la Afrika kupata hasara ya mabilioni ya dola kutokana na utajiri wa Afrika kuondolewa kinyume cha sheria barani humo.
Thabo Mbeki ameyasema hayo katika mkutano na waandishi habari mjini Johannesburg na kutangaza kuwa bara la Afrika hupata hasara ya takribani dola bilioni 80 kutokana na kuhamishiwa nje utajiri wa bara hilo.
Kwa mujibu wa takwimu ambazo Mbeki amewasilisha, utajiri unaohamishwa kutoka Afrika ni juu zaidi ya kiwango kinachotajwa na Shirika la Kimataifa la Fedha IMF.
Kwa mujibu wa IMF, kila mwaka bara la Afrika hupoteza dola bilioni 50 ambazo hupelekwa nje ya bara hilo kinyume cha sheria.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini aidha amezitaka serikali za Afrika kuimarisha zaidi mfumo wa ukusanyaji kodi kwani kuna upungufu mkubwa katika mfumo wa kodi barani humo.
Thabo Mbeki ni mwenyekiti wa jopo la Umoja wa Afrika kuhusu kuondolewa kinyume cha sheria utajiri wa Afrika.