Waliofariki dunia katika ajali ya ndege Sudan Kusini wafika 17
Watu wasiopungua 17 wamepoteza maisha baada ya ndege ya mizigo kuanguka, muda mfupi baada ya kupaa angani ikitokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Juba nchini Sudan Kusini.
Waziri wa Uchukuzi wa Sudan Kusini, Madit Biar Yel amethibitisha habari ya kutokea ajali hiyo ya ndege ya mizigo ya shirika la South West Aviation mapema jana Jumamosi.
Kur Kuol, Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Juba amesema ndege hiyo ilikuwa inaelekea katika maeneo ya Aweil na Wau kuwafikishia mishahara wafanyakazi wa shirika moja.
Ameongeza kuwa, uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali hiyo umeanzishwa.

Duru za habari zinasema kuwa, mtu mmoja tu ndiye aliyenusurika kwenye ajali hiyo na hivi sasa anaendelea kutibiwa hospitalini.
Itakumbukwa kuwa, watu 17 waliuawa katika ajali nyingine ya ndege ya shirika la South West mashariki mwa eneo la Lakes Regions nchini Sudan Kusini mwaka 2018.