Wanamgambo wa ADF waua watu 20 mashariki mwa DRC
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limetangaza kuwa wanamgambo wa kundi la ADF wameuwa raia 20 katika hujuma dhidi ya vijiji vitatu mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa zinasema maafisa wa usalama wamepata maiti za watu waliouawa leo Jumatano katika vijiji vya Mapasana, Mayitike na Sayuni, yapata kilomita 30 kaskazini maghairbi mwa mji wa Beni.
Mauaji hayo yamefanyika siku tatu tuu baada ya hujuma kama hiyo iliyopelekea watu 13 kupoteza maisha.
Waasi wa Uganda wa Allied Democratic Forces (ADF) wako mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwaka 1994 ambako wamekuwa wakifanya jinai na hujuma mbalimbali dhidi ya raia wa eneo hilo. Katika kipindi cha miaka hiyo yote waasi hao wameua mamia ya watu katika eneo la Beni.

Mwaka jana jeshi la DRC lilianzisha oparesheni kubwa dhidi ya ADF na kundi hilo nalo limekuwa likitekeleza hujuma za kulipiza kisasi dhidi ya raia. Umoja wa Mataifa unasema yanayojiri katika eneo hilo yamkini yakatambuliwa kuwa ni jinai za kivita.
Kushindwa jeshi la Kongo na kikosi cha MONUSCO kukabiliana na wanamgambo wenye silaha wakiwemo waasi hao kumepelekea kushtadi ukosefu wa amani nchini humo khususan mashariki mwa nchi.