50 waaga dunia baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63379-50_waaga_dunia_baada_ya_mgodi_wa_dhahabu_kuporomoka_kongo_dr
Kwa akali watu 50 wamepoteza maisha baada ya kuporomokewa na mgodi wa dhahabu karibu na mji wa Kamituga, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 12, 2020 07:00 UTC
  • 50 waaga dunia baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka Kongo DR

Kwa akali watu 50 wamepoteza maisha baada ya kuporomokewa na mgodi wa dhahabu karibu na mji wa Kamituga, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Duru za habari zinaarifu kuwa, mgodi huo ulioko katika mkoa wa Kivu Kusini uliporomoka jana Ijumaa kutokana na mvua kubwa zilizoshuhudiwa nchini humo. Nchi kadhaa za Afrika zinashuhudia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha kwa wiki kadhaa sasa.

Ajali za namna hii hususan katika migodi ya dhahabu huko DRC zimekuwa zikishuhudiwa mara kwa mara kutokana na usimamizi mbaya wa uchimbaji madini na magendo ya madini zenye thamani.

Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka jana, watu 43 waliaga dunia katika maporomoko mengine yaliyotokea kwenye mgodi wa dhahabu unaosimamiwa na kampuni ya Glencore yenye makao makuu yake mjini Baar nchini Uswisi huko Kongo DR.

Wachimbaji migodi wa Kiafrika waendelea kuishi kwa umaskini wa kupindukia licha ya kuhatarisha maisha yao

Aidha Oktoba mwaka jana, wachimba migodi 16 wamefariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi wa dhahabu huko mashariki mwa nchi hiyo.

Takwimu zinaonyesha, aghalabu ya madini hususan ya dhahabu na almasi yanayochimbwa kinyume cha sheria Kongo DR, Chad miongoni mwa nchi nyingine za Afrika, husafirishwa kimagendo katika nchi za Ulaya na Uarabuni.