Guterres: Machafuko ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanatia wasiwasi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63418-guterres_machafuko_ya_mashariki_mwa_jamhuri_ya_kidemokrasia_ya_congo_yanatia_wasiwasi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kutokana na ghasia na machafuko yanayoongezeka kila uchao katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 14, 2020 04:38 UTC
  • Antonio Guterres
    Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kutokana na ghasia na machafuko yanayoongezeka kila uchao katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Antonio Guterres amesema Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa kutokana na machafuko yaliyosababisha vifo vya makumi ya raia katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri katika siku chache za hivi karibuni.

Taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imesisitiza kuwa, umoja huo unabeba jukumu la kuwalinda raia na serikali ya Congo DR katika jitihada za kuimarisha amani na utulivu mashariki mwa nchi hiyo. 

Antonio Guterres pia amesema Umoja wa Mataifa unaunga mkono juhudi za maafisa wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo za kuwafikisha mahakamani watu walioshambulia raia na askari wa kulinda amani wa kikosi cha umoja huo cha MONUSCO. 

Wapiganaji wa kundi la waasi la ADF kutoka Uganda Jumanne na Jumatano ya wiki iliyopita walishambulia vijiji vya mkoa wa Ituri na kuua watu wasiopungua 58. 

Waasi wa ADF

Waziri wa Mambo ya Ndani wa DRC, Adjio Gidi amesema kuwa, idadi kubwa ya watu katika maeneo yaliyoshambuliwa wamekimbia makazi yao wakihofia usalama wa maisha yao.

Amesema, "ADF iliua watu 23 katika eneo la Irumu kusini mwa mkoa wa Ituri Jumanne na kisha ikaua watu wengine 35 katika eneo hilo siku iliyofuatia. 

Mkazi mmoja wa kijiji chenye misitu mikubwa cha Tshabi katika mkoa wa Ituri amenukuliwa na duru za habari akisema kuwa, wanamgambo hao walitumia bunduki, visu, mapanga na silaha nyinginezo katika mashambulio hayo ya Jumanne na Jumatano.