Sep 19, 2020 12:47 UTC
  • Magaidi 16 wa Boko Haram waangamizwa na jeshi la Nigeria

Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuuawa wanachama 16 wa kundi la kigaidi la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

John Enenche, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Nigeria amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu la Uturuki akisema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, magaidi hao waliuawa katika shambulizi la anga katika kijiji cha Kassa Kura mjini Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno lililoathiriwa zaidi na mashambulizi ya Boko Haram.

Eneche amesema wanachama kadhaa wamekimbia wakiwa na majeraha ya risasi baada ya shambulizi hilo. Ameongeza kuwa, magaidi 11 wametiwa mbaroni katika operesheni hiyo, mbali na kunaswa shehena ya silaha ya magaidi hao.

Mapema mwezi huu, watu wasiopungua 10 waliuawa katika shambulizi la kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika mji huo wa Maidugiri, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Magaidi wa Boko Haram

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram lilibeba silaha na kuanzisha uasi mwaka 2009 kwa lengo la kuasisi utawala eti wa Kiislamu kaskazini mwa Nigeria, ambapo mbali na ndani ya nchi hiyo, limepanua wigo wa mashambulio yake katika nchi jirani pia za Niger, Chad na Cameroon.

Zaidi ya watu 20 elfu wameuawa katika nchi hizo nne za magharibi mwa Afrika na zaidi ya wengine milioni mbili wamekuwa wakimbizi baada ya kulazimika kuyahama makazi yao.

Tags