Sep 23, 2020 13:20 UTC
  •  Ongezeko la vitendo vya kigaidi lapelekea raia wa Msumbiji 310,000 kuhama makazi yao

Ongezo la vitendo vya uasi vya wanamgambo wenye silaha kaskazini mwa Msumbiji limesababisha mamia ya maelfu ya watu kuyahama makazi yao.

Waasi hao wamezidisha mashambulizi katika wiki za karibuni katika mkoa wa Cabo Delgado na kuiteka bandari ya kiistratijia ya Mocimboa da Praia. Waasi hao waliidhibiti bandari hiyo kwa wiki sita.  

Mapigano kati ya wanamgambo wenye silaha na wenye misimamo ya kuchupa mipaka na vikosi vya serikali ya Msumbiji yamezusha hofu miongoni mwa raia na kuwafanya wakimbie makazi yao.

Wanamgambo wenye mfungamano na Daesh katika mkoa wa Cabo Delgado, Msumbiji  

Mpango wa Chakula Duniani (WFP) jana Jumanne ulitangaza kuwa wimbi hilo la raia wanaohama makazi yao huko kaskazini mwa Msumbiji linasababisha maafa na kulifanya suala la kuwasaidia haraka watu hao kuwa jambo la dharura la kibinadamu.

Lola Castro Mkurugenzi wa WFP wa kanda hiyo ameeleza kuwa, hivi sasa kuna jumla ya watu 310,000 katika mkoa wa Cabo Delgado, Nampula na Niassa waliokimbia makazi yao. UNHCR pia imeripoti kuwa, wakimbizi wapatao laki moja wamevuka Mto Ruvuma na kuingia Tanzania.  

Watu zaidi ya 1,500 wameuliwa tangu kuanza machafuko huko Cabo Delgado mwaka 2017. Kundi hilo la wanamgambo lililotangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi na Daesh yaani ISIS na vikosi vya serikali ya Msumbiji wote wanatuhumia kuhusika na jinai hizo.

Tags