Mafuriko yasababisha watu laki sita kukosa makazi Sudan Kusini
(last modified Sat, 26 Sep 2020 02:46:48 GMT )
Sep 26, 2020 02:46 UTC
  • Mafuriko yasababisha watu laki sita kukosa makazi Sudan Kusini

Mafuriko makubwa huko Sudan Kusini yamesababisha watu zaidi ya laki sita kuhama makazi yao tangu mwezi Julai mwaka huu. Umoja wa Mataifa jana Ijumaa ulitoa tahadhari baada ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwa miezi kadhaa sasa kusababisha kingo za Mto Nile kupasuka.

Nchi hiyo maskini mbali na kukumbwa na mafuriko hayo inasumbuliwa pia na uhaba mkubwa wa chakula tangu zamani. Wataalamu wa mazingira wanasema kuwa mvua zisizo za kawaida zinasababishwa na mzungumko wa hali ya hewa uliotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Alain Noudehou Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mafaifa nchini Sudan Kusini ameeleza kuwa, mafuriko hayo makubwa yaliyoiathiri nchi hiyo yanakwamisha juhudi mbalimbali za utoaji misaada, huku familia zikilazimika kujikusanya pamoja huku kukiwa hakuna ardhi ya kutosha ya kuanzisha kliniki na shule.

Ameongeza kuwa hadi sasa Umoja wa Mataifa umetenga dola milioni 10 ili kuwasaidia wahanga wa mafuriko hata hivyo unahitaji fedha zaidi ya dola milioni 40 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu. 

Wakati huo huo mwezi uliopita Sudan, nchi jirani na Sudan Kusini pia ilikumbwa na mafuriko makubwa. 

Mafuriko katika mto Blue Nile nchini Sudan 

Maafisa wa Sudan walitangaza kuwa nchi hiyo imepata hasara na maafa makubwa ya mali na roho za watu kutokana na kufurika Mto Nile nchini humo.

Kujaa pomoni maji ya mto huo ambako kulisababishwa na mvua kubwa zilizonyesha mwezi uliopita huko Sudan kumesababisha makumi ya watu kufariki dunia na maelfu ya wengine kupoteza makazi yao.