WFP: Wahanga wa mafuriko Sudan Kusini wanahitaji misaada
Mvua kubwa za msimu ambazo zimesababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali huko Sudan Kusini zimewaathiri watu zaidi ya laki saba nchini humo.
Watu hao walioathiriwa na mafuriko aidha wanakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana ulisababishwa na mashambulio ya nzige huku wakikabiliwa pia na maambukizi ya Covid-19.
Habari zinasema kuwa maeneo mengi ya Sudan Kusini yako chini ya maji huku Mto Nile ukiwa umefika katika kiwango cha juu kabisa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 50.
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umekuwa ukigawa misaada ya chakula kwa watu zaidi ya laki tano katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko huko Sudan Kusini huku tishio la ukame nchini humo likiongezeka.
Hali ya kibinadamu huko Sudan Kusini inazidi kuwa mbaya kutokana na kuendelea kunyesha mvua hizo za msimu na kutokea mafuriko yanayokwamisha usambazaji wa chakula kwa raia.

Peter Smerdon Msemaji wa WFP anasema: Sudan Kusini inakabiliwa na hali ngumu kwa sababu ya mzozo wa ndani na idadi kubwa ya watu kupoteza makazi yao. Nchi wafadhili zinapasa kuchukua hatua kuisaidia nchi hiyo. Amesema hata hivyo nchi wafadhili zenyewe hivi sasa zinahangaika pia kupambana na maradhi ya Covid-19; kwa hiyo ni vigumu kutoa msaada katika kipindi hiki kigumu sana.