Sep 30, 2020 12:47 UTC
  • Rais wa zamani wa Sierra Leone azuiwa kuondoka nchini, kisa ufisadi

Serikali ya Sierra Leone imemuwekea vikwazo vya kusafiri nje ya nchi aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Ernest Bai Koroma anayeandamwa na tuhuma za ufisadi wa kifedha.

Koroma pamoja na watu wengine zaidi ya 100 waliohudumu katika enzi za utawala wa kiongozi huyo hawatoruhisiwa kuondoka nchini humo, na wametakiwa kurejesha fedha walizofuja katika hazina ya nchi, mbali na kukabidhi nyumba zao kwa mamlaka husika, la sivyo waendelee kufanyiwa uchunguzi zaidi. 

Hata hivyo chama cha upinzani cha rais huyo wa zamani wa Sierra Leone cha All People's Congress (APC) kimekanusha madai hayo ya wizi wa fedha za umma. Mmoja wa mawakili wa chama hicho amesema wataenda mahakamani kukata rufaa ya kupinga marufuku hiyo ya kusafiri nje ya nchi.

Rais wa Sierra Leone, Julius Maada Bio

Wiki iliyopita, Rais wa sasa wa nchi hiyo, Julius Maada Bio alisema tangazo la Kamisheni ya Uchunguzi inayoongozwa na majaji wa kigeni lina umuhimu mkubwa kwa kuwa litaufanya ufisadi uonekana ni hatari. Amebainisha kuwa, taifa hilo halitaruhusu ufisadi wa namna hiyo ilhali linataka listawi. 

Hii ni katika hali ambayo, nara na kaulimbiu ya Ernest Bai Koroma katika kampeni za uchaguzi wa urais wa mwaka 2007 ilikuwa ni mabadiliko na kufanya harakati kuelekea kwenye uboreshaji wa maisha ya raia.

Koroma na waitifaki wake katika chama kilichokuwa kinatawala wakati huo wamekuwa wakituhumiwa kuwa walitumia vibaya fedha za miradi mikubwa ya kiuchumi kutoka nchi za Magharibi.

Tags