Mahasimu Sudan Kusini waahidi kutekeleza makubaliano ya amani
(last modified Wed, 14 Oct 2020 07:55:18 GMT )
Oct 14, 2020 07:55 UTC
  • Mahasimu Sudan Kusini waahidi kutekeleza makubaliano ya amani

Serikali ya Sudan Kusini na makundi ya upinzani zimeahidi kwa mara nyingine kufuata Makubaliano ya Kusitisha Uhasama (COHA) katika mazungumzo ya amani yaliyomalizika hivi karibuni huko Rome.

Kiongozi wa ujumbe wa serikali ya Sudan Kusini Barnaba Marial Benjamin amesema, wamekubaliana na makundi ya upinzani yaliyoongozwa na Muungano wa Harakati za Upinzani (SSOMA) kuhusu kufuata makubaliano ya kusitisha mapambano yaliyosainiwa mwezi Januari kabla ya kuanza kwa raundi ijayo ya mazungumzo kuhusu chanzo cha mogogoro nchini Sudan Kusini.

Ameongeza kuwa, pande hizo mbili zitafanya tena mazungumzo tarehe 30 mwezi Novemba, ili kuendelea na majadiliano kuhusu masuala ya kisiasa ambayo ndio chanzo cha mgogoro nchini humo.

Marial amesema mazungumzo ya Roma hayakugusia kadhia ya mipaka ya majimbo au marekebisho ya katiba kama ilivyopendekezwa na wapinzani. Amesema bunge la mpito ndilo litakalojadili kuhusu katiba mpya baada ya kuanza shughuli zake.

Muungano wa Harakati za Upinzani (SSOMA) nao umetoa taarifa na kusema unafungamana na mapatano hayo ya Roma kabla ya duru ijayo ya mazungumzo.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini (kulia) na hasimu wake mkuu Riek Machar

Nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ilitumbukia kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu makamu wake wakati huo, Riek Machar kuwa alipanga njama ya kumpindua. 

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kwa kupiga kura ya maoni iliyoungwa mkono na asilimia 99 ya raia wake baada ya vita vya miongo kadhaa vya kupigania kujitenga. Inasadikiwa kuwa Sudan Kusini ilichochewa na madola ya kibeberu kujitenga na Sudan.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimeshababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.