ADF yaua watu wasiopungua 19 Mashariki mwa Congo DR
Kundi moja la kutetea haki za binadamu limetangaza kuwa watu wasiopungua 19 wameuawa katika shambulizi lililofanywa na waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ripoti zinasema mauaji hayo yamefanyika katika kijiji cha eneo la Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limethibitisha kutokea mauaji hayo bila ya kutoa maelezo zaidi.
Raia wa meneo hayo wanavilaumu vikosi vya jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa kwamba, havitekelezi majuku yake ya kulinda usalama na maisha ya raia, na badala wake askari hao wanatumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na waandamanaji.
Kundi la waasi kutoka Uganda la Allied Democratic Forces (ADF) limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki mwa Congo DR tangu muongo wa 90.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, kundi hilo limeua raia zaidi ya elfu moja tangu mwaka jana 2019 hadi hivi sasa.