Makada 20 wa CHADEMA kizimbani kwa kuchochea maandamano Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64402-makada_20_wa_chadema_kizimbani_kwa_kuchochea_maandamano_tanzania
Jeshi la Polisi mkoani Singida katikati mwa Tanzania limewafikisha mahakamani viongozi na wafuasi 20 wa chama cha upinzani cha CHADEMA kwa tuhuma za kukusanyika na kufanya kikao kinyume cha sheria, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kufanya vurugu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 03, 2020 07:31 UTC
  • Makada 20 wa CHADEMA kizimbani kwa kuchochea maandamano Tanzania

Jeshi la Polisi mkoani Singida katikati mwa Tanzania limewafikisha mahakamani viongozi na wafuasi 20 wa chama cha upinzani cha CHADEMA kwa tuhuma za kukusanyika na kufanya kikao kinyume cha sheria, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kufanya vurugu.

Kadhalika viongozi kadhaa hadi sasa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai kuwa maandamano waliyoyaitisha yana nia ya kuibua vurugu na ghasia nchini humo.

Huku hayo yakijiri, aliyekuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CHADEMA, Tundu Lissu ambaye alikamatwa na polisi jana jioni ameachiwa bila masharti baada ya mahojiano na Polisi. Lisu ameachiwa yeye na aliokuwa ameambatana nao.  

Siku ya Jumamosi, viongozi wa CHADEMA na wa ACT Wazalendo walitoa tamko la pamoja la kuitisha maandamano ya amani yasiyo na kikomo kuanzia jana, ya kudai uchaguzi mpya na tume huru ya uchaguzi baada ya kuyakataa rasmi matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 28 uliokipa ushindi wa kishindo chama tawala CCM.

Tundu Lissu

 

Vyama hivyo vimedai kuwa kilichofanyika Oktoba 28 ni unyang'anyi na uporaji wa kutumia nguvu wa haki ya Watanzania ya kuwachagua viongozi wanaowataka kwa njia ya demokrasia uliofanywa kwa makusudi na tume zote mbili za uchaguzi Tanzania za NEC na ZEC, vyombo vya ulinzi vya usalama na makundi ya wahalifu yanayoratibiwa, kuongozwa na kulindwa na vyombo vya usalama. Hata hivyo madai hayo yamekanushwa na vyombo hivyo.

 Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza mgombea urais wa Tanzania Bara kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), John Pombe Magufuli kuwa ndiye mshindi wa kinyang'anyiro hicho baada ya kupata kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4 ya kura zote halali zilizopigwa. Hapo jana, Dakta Hussein Ali Mwinyi aliapishwa kuwa Rais wa nane wa Zanzibar katika hafla kubwa iliyofanyika visiwani Zanzibar, baada ya kushinda uchaguzi wa rais kupitia CCM.