UN: Hali ya wakimbizi wa Ethiopia nchini Sudan inatia wasiwasi
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa una wasiwasi kuhusu hali ya wakimbizi wa Ethiopia wanaoendelea kumiminika katika nchi jirani ya Sudan iwapo raia zaidi watalazimika kukimbia mapigano yanayojiri kati ya jeshi la Serikali Kuu ya Ethiopia na wapiganaji wa Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (The Tigray People's Liberation Front (TPLF)) huko kaskazini mwa Ethiopia.
Ann Encontre, mwakilishi wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) nchini Ethiopia amesema kuwa UN inajadiliana na pande mbili zinazozozana kwa ajili ya kufungua njia ya misaada ya kibiandamu.
Amesema kuwa usafirishaji hauruhusiwi kwenda na kutoka Tigray, na kwa sababu hiyo kumeripotiwa ukosefu wa bidhaa za kimsingi, suala ambalo limeathiri matabaka dhaifu ya jamii.
Vilevile mashirika ya misaada yameeleza wasiwasi wao kuhusu usalama wa watoto, wanawake, wazee na walemavu, kutoka na mapigano yanayoendelea baina ya jeshi la Ethiopia na kundi la TPLF.
Sudan imepokea zaidi ya wakimbizi 10,000 wa Ethiopia tangu mapigano yalipoanza katika eneo la Tigray, na mashirika ya misaada yanasema kuwa yameishiwa na akiba ya chakula, dawa na vifaa vingine vya dharura.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Ahmed Abiy leo Alhamisi amesema jeshi la nchi hiyo limekomboa sehemu ya magharibi ya mkoa wa Tigray ambako wanajeshi wa Shirikisho wamekuwa wakipambana na wapiganaji wa Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray.
Tarehe 4 mwezi huu Jeshi la Ethiopia lilianza mashambulizi dhidi ya Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (The Tigray People's Liberation Front (TPLF)).
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alisema kuwa, serikali yake imejaribu kuepuka vita na mapigano lakini jambo hilo haliwezi kufanywa na upande mmoja.