Sudan yakanusha kupiga kura kwa manufaa ya Israel katika Umoja wa Mataifa
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imetoa taarifa na kukanusha taarifa zilizosambazwa na vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vilivyodai kwamba Khartoum imepiga kura kwa manufaa ya Israel katika Umoja wa Mataifa.
Mtandao wa habari wa al Yaum al Sabi'i umeinukuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ikisema siku ya Jumatano kwamba taarifa zilizoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari ya kwamba Khartoum imepiga kura kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa, hazina ukweli wowote.
Taarirfa hiyo imeongeza kuwa, Sudan haijawahi kupiga kura kwa manufaa ya Israel katika kikao chochote cha hivi karibuni wala vya huko nyuma vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Gazeti la Kizayuni la Israel Hayom ndilo lililoeneza madai hayo na kusema kuwa Sudan imeunga mkono na kupigia kura ya ndio mpango uliopendekezwa na Israel katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Tarehe 23 Oktoba 2020, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilitangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel chini ya usimamizi wa Marekani.
Sudan ilifuata mkumbo wa Imarati na Bahrain katika kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao mikono yake inachiriza damu za Waislamu na Waarabu wa Palestina. Kabla ya hapo nchi za Misri na Jordan nazo ziliwahi kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel.
Hadi hivi sasa wananchi, vyama na makundi ya kisaisa na wanaharakati mbalimbali wa Sudan wanaendelea kutangaza waziwazi kuchukizwa na hatua hiyo ya serikali ya mpito ya Khartoum; ya kutangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni.