Bunge DRC lapiga kura ya kumtimua spika aliyekuwa akimuunga mkono Kabila
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65128-bunge_drc_lapiga_kura_ya_kumtimua_spika_aliyekuwa_akimuunga_mkono_kabila
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jeanine Mabunda ametimuliwa katika nafasi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 11, 2020 03:42 UTC
  • Bunge DRC lapiga kura ya kumtimua spika aliyekuwa akimuunga mkono Kabila

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jeanine Mabunda ametimuliwa katika nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa  wabunge waliowengi wamepiga kura ya kumtimua Mabunda ambaye ni kutoka chama cha rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Kabila. Hatua hiyo inaashiria kupata nguvu mrengo wa Rais Felix Tshisekedi katika bunge.

Kwa mujibu wa taarifa katika upigaji kura wa Alhamisi jioni, wabunge 281 waliunga mkono kuuzuliwa Mabunda huku 200 wakipinga. Bunge hilo lina wabunge 500.

Wabunge wamemtuhumu Mabunda kuwa uongozi wake ulikuwa mbovu kwani alipendelea chama chake na hakuwa na uwazi katika usimamizi wa masuala ya kifedha. Mabunda alikanusha tuhuma dhidi yake huku akiomba radhi. Hata hivyo wabunge waliowengi walipiga kura ya kumtimua.

Joseph Kabila (kushoto) na  Félix Tshisekedi

Kilichowashangaza wengi ni kuwa spika huyo ameshindwa kupata kura za kutosha kumtetea wakati wabunge wa chama chake cha FCC ndio wengi zaidi bungeni.

Hayo yanajiri wakati ambao Jumapili Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, alitangaza kuweka mpango wa kuvunja serikali ya muungano na chama cha aliyekuwa rais wa nchi, Joseph Kabila.

Tshisekedi anasema ameshindwa kutekeleza matakwa ya Wakongo kwa kipindi cha miaka miwili kutokana na changamoto katika muungano huo.