Shahriari: Kujitolea mhanga Sheikh Zakzaky kumevunja njama za maadui
Katibu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu amesema kuwa, kujitolea muhanga Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambaye anashikiliwa kizuizini kwa miaka kadhaa sasa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo kumevuruga na kuvunja njama za maadui.
Sheikh Hamid Hawali Shahriari amesema hayo kwa mnasaba wa kumbukumbuu ya mauaji ya Zaria yaliyotokea mwaka 2015 na kusisitiza kuwa, kimya cha taasisi za kimataifa mkabala wa mauaji ya Zaria kinadhihirisha undumakuwili wa asasi hizo na namna zinavyolitimaza suala la haki za binadamu.
Amesema, "kukamatwa kwa Sheikh Zakzaky kiongozi wa Waislamu wa Kishia, kuuawa idadi kubwa ya wafuasi wake akiwemo mtoto wa kiongozi huyo, mashambulizi ya mara kwa mara ya jeshi la Nigeria dhidi ya makazi wa Mashia wa Zaria, kuuawa viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, kushambuliwa makao makuu ya Mashia katika miji ya Sokoto na Zaria, na madai yasiyo na msingi ya jeshi la nchi hiyo kuwa harakati hiyo inapanga njama za kumuua kamanda wa jeshi, yote hayo yanaashiria njama zilizoratibiwa na Wazayuni."
Vile vile Katibu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu amesema mauaji ya halaiki ya Waislamu wa Zaria ni mfano hai wa ukatili wa madhalimu ambao hawakubali kabisa kuona umma wa Kiislamu ukiwa na umoja na mshikamano.
Juzi Jumamosi Waislamu wa Nigeria walikumbuka mauaji ya kutisha yaliyofanywa na jeshi la nchi hiyo katika mji wa Zaria jimboni Kaduna miaka mitano iliyopita, huku serikali ya Rais Muhamadu Buhari ikiwa imekataa kumuachilia huru Sheikh Zakzaky, licha ya mahakama kutoa amri ya kuachiliwa huru kiongozi huyo wa Kiislamu.
Katika shambulio la Disemba 12, 2015, inakadiriwa wanachama zaidi ya 1,000 wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, aghalabu wakiwa ni Waislamu wa madhehebu ya Shia waliuawa kwa kufyatuliwa risasi na jeshi la Nigeria.