Machar atoa wito wa maelewano Sudan Kusini
(last modified Thu, 17 Dec 2020 11:57:49 GMT )
Dec 17, 2020 11:57 UTC
  • Machar atoa wito wa maelewano Sudan Kusini

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini Bw. Riek Machar ametoa wito wa kuanza mchakato wa upatanishi nchini humo, ili kuwaunganisha watu na kuleta maelewano ili kutekeleza mapatano ya amani ya 2018.

Katika taarifa aliyoitoa kwa mnasaba wa kukumbuka kuanza kwa vita vya mwaka 2013 nchini humo, Machar amesema wakati umefika sasa wa kurejesha amani, uadilifu na uthabiti Sudan Kusini. Amesema hatua zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa nchi hiyo haitumbukii tena katika ghasia na machafuko.

Machar anayeongoza chama cha upinzani cha SPLM-IO ambacho kimegawana madaraka na chama cha SPLM kinachoongozwa na Rais Salva Kiir, amesema serikali ya mpito itaanzisha mchakato wa upatanishi.

Nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ilitumbukia kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu makamu wake wakati huo, Machar kuwa alipanga njama ya kumpindua.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kwa kupiga kura ya maoni iliyoungwa mkono kwa wingi na raia wa eneo hilo baada ya vita vya miongo kadhaa vya kupigania kujitenga. Inasadikiwa kuwa Sudan Kusini ilichochewa na madola ya kibeberu kujitenga na Sudan.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

Pande zote katika mapatano mapya ya amani ya Sudan Kusini zimeahidi kwa mara nyingine kuheshimu Makubaliano ya Kusitisha Uhasama (COHA) katika mazungumzo ya amani yaliyomalizika hivi karibuni huko Rome.