Uingiliaji wa kigeni nchini Libya; chanzo cha kuvunjika mazungumzo ya amani
(last modified Fri, 18 Dec 2020 02:49:18 GMT )
Dec 18, 2020 02:49 UTC
  • Uingiliaji wa kigeni nchini Libya; chanzo cha kuvunjika mazungumzo ya amani

Uingiliaji wa nchi za nje katika masuala ya ndani ya Libya unaendelea katika hali ambayo duru mpya ya mazungumzo ya amani ya nchi hiyo imevunjika kutokana na tofauti zilizoibuka kuhusu namna ya kuwachagua wanachama wa baraza la mawaziri.

Kuhusu suala hilo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia katika kikao chake cha siku ya Jumanne liliwataka mamluki na wale wote wanaobeba silaha kinyume cha sheria waondoke katika ardhi ya Libya mara moja.

Ni muda sasa ambapo Libya inashuhudia mgogoro mkubwa wa ndani. Kuwepo serikali mbili hasimu katika nchi hiyo na kuungwa mkono serikali hizo na nchi za nje ni jambo ambalo zimezidisha mgogoro huo wa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Hivi sasa kuna askari wa kigeni katika ardhi ya Libya ambao wametumwa huko kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja. Uturuki, Qatar, Algeria, Italia na Umoja wa Ulaya zinaunga mkono serikali inayoongozwa na Fayez al-Sarraj katika hali ambayo Misri, Imarati na Saudi Arabia ni waungaji mkono wakuu wa wapiganaji wa Jenerali muasi Khalifa Haftar.

Askari wa Uturuki nchini Libya

Uturuki imetuma Libya mamluki wake wa kigaidi kutoka Syria nazo Imarati na Saudi Arabia zimetuma nchini humo mamluki wao wa vita kutoka Sudan na hivyo kuzifanya nchi hizo kuwa washiriki wakubwa katika vita vinavyochochewa na nchi za kigeni katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Suala hilo si tu kwamba limeongeza uwezekano wa kugawanywa Libya vipande vipande bali pia linaifanya nchi hiyo kuwa kituo muhimu cha makundi ya kigaidi kieneo.

Wasiwasi wa kuongezeka mgogoro huo umezifanya baadhi ya nchi na taasisi za kimataifa kujaribu kuingilia kati kwa ajili ya kupatanisha pande zinazohasimiana huko Libya. Juhudi hizo zimepelekea kufanyika duru kadhaa za mazungumzo ya amani baina ya makundi ya nchi hiyo. Pamoja na hayo lakini duru mpya ya mazungumzo ya karibuni kwa ajili ya kuwateua wanachama wa baraza la mawaziri imemalizika bila mafanikio yoyote na hivyo kuongeza wasiwasi wa kukiukwa usitishaji vita na kuanza mapigano mapya ya ndani.

Pamoja na kufanyika mazungumzo hayo ya amani, lakini uingiliaji wa kigeni nao umekuwa ukiendelea. Uturuki na Imarati ni nchi mbili muhimu zinazohusika katika mapigano ya kieneo huko Libya. Uturuki inaendelea kutuma Libya silaha na zana za kivita kwa mujibu wa mapatano ya kijeshi, kiusalama na masuala ya bahari yaliyofikiwa kati ya Ankara na Tripoli. Katika upande wa pili Misri na Imarati nazo zimeongeza misaada yao ya kijeshi kwa Jenerali Haftar, jambo ambalo limeamsha malalamiko mengi ndani ya Libya.

Mamluki wa Sudan katika vita vya Libya

Kuhusu hilo, as-Swadiq al-Gharyani, Mufti wa Lbya hivi karibuni alilaani uingiliaji wa Imarati nchini kwake na kusema kuwa Imarati ni muuaji wa watu wa Libya.

Kwa vyovyote vile juhudi za kutatua mgogoro wa Libya zingali zinaendelea kama ambavyo kuteuliwa kwa mjumbe mpya maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya Libya na sisitizo lake la kudumishwa mazungumzo ya amani ni jambo linalotia matumaini kwamba huenda njia ya kutatuliwa mgogoro huo ikapatikana karibuni. Wengi wanasubiri kuona matokeo ya jitihada zitakazofanywa na mjumbe huyo kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Libya lakini pamoja na hayo ushahidi uliopo unaonyesha kuwa hakuna lolote la maana linalofanyika katika uwanja huo.

Faisal as-Shariff, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema kuhusu suala hilo kwamba kuingia kwa sura mpya, yaani Nikolai Mladinov, katika mgogoro wa Libya kamwe hakutakuwa na matokeo chanya yanayotarajiwa.

Ni wazi kuwa, mapatano rasmi ya kutatua mgogoro wa Libya yatafikiwa tu pale uingiliaji wa kigeni katika nchi hiyo utakapokomeshwa na nchi jirani kuchukua jukumu la kulinda amani katika mipaka yao ili isitumiwe na makundi ya kigaidi kuingia Libya. Jambo hilo linaonekana kuwa mbali kufikiwa kwa sasa kwa kutilia maanani utajiri mkubwa wa Libya na hitilafu za kisiasa zilizopo nchini humo.