Jeshi la Sudan latoa onyo kali kwa Ethiopia
Jeshi la Sudan limesema litatoa jibu kwa hatua za kuvuruga amani katika maeneo ya mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Ethiopia.
Gazeti la Al Qudsul-Araby limeripoti kuwa jeshi la Sudan limeeleza katika taarifa kuhusiana na mapigano kati yake na askari wa Ethiopia katika mpaka wa pamoja wa nchi mbili kwamba, mpaka wa Sudan na Ethiopia unafahamika vyema.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, mipaka ya kimataifa kati ya Sudan na Ethiopia inajulikana vyema, wala hakuna mjadala na mabishano yoyote kuhusu suala hilo, kwa hivyo jeshi la Sudan litasonga mbele hadi nukta ya mwisho kabisa ya mpaka huo na wala halitafumbia macho kuchukua hatua kuhakikisha ardhi yote ya Sudan inakuwa chini ya udhibiti na ulinzi wake.
Siku ya Jumatano iliyopita, jeshi la Sudan lilitangaza kuwa, vikosi vyake vimeshambuliwa na jeshi la Ethiopia katika eneo moja la mpaka wa pamoja linalozozaniwa na nchi hizo.
Katika upande mwingine, na baada ya Sudan kutuma zana za kivita katika mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Ethiopia, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ametaka balozi wa Sudan nchini humo atoe maelezo kuhusu sababu za hatua hiyo ya Khartoum.
Juzi Alkhamisi pia, Waziri Mkuu wa Ethiopia aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, harakati za wanamgambo wa kieneo katika mpaka wa Ethiopia na Sudan zinafuatiliwa kwa karibu. Hata hivyo alisema, matukio hayo hayatoharibu uhusiano wa nchi hizo mbili kwani Ethiopia muda wote inaamini kwamba mazungumzo ndiyo njia pekee ya kutatua matatizo yanayojitokeza.../