Jeshi la Ethiopia lalipiza kisasi, laua wabeba silaha 42 mpakani na Sudan
(last modified Fri, 25 Dec 2020 13:15:04 GMT )
Dec 25, 2020 13:15 UTC
  • Jeshi la Ethiopia lalipiza kisasi, laua wabeba silaha 42 mpakani na Sudan

Watu 42 waliokuwa wamebeba silaha wameuawa na wanajeshi wa Ethiopia katika eneo la Benishangul-Gumuz, magharibi mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, mpakani na Sudan.

Kwa mujibu wa televisheni ya serikali ya Fana, watu hao wasiojulikana na wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya watu zaidi ya 100 katika kijiji kimoja kilichoko katika eneo la Benishangul-Gumuz waliuawa jana Alkhamisi katika operesheni ya jeshi la Ethiopia.

Serikali ya Addis Ababa tayari imetuma askari zaidi katika eneo hilo kwa ajili ya kushika doria na kudhibiti mapigano ya kikabila katika eneo hilo. Jana Alkhamisi, Waziri Mkuu wa Ethipia, Abiy Ahmed alisema serikali yake imetuma maafisa usalama katika eneo la Benishangul-Gumuz, mpakani na Sudan, siku moja baada ya makumi ya wanakijiji kuuawa katika shambulio la wabeba silaha. 

Kwa mujibu wa Tume ya Haki za Binadamu Ethopia, watu 100 waliuawa katika kijiji cha Bekoji katika wilaya ya Bulen baada ya wanamgambo kuwashambulia wakiwa wamelala mapema Jumatano, mbali na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Eneo la Benishangul-Gumuz la Ethiopia, mpakani na Sudan

Eneo hilo ni makazi ya makabila kadhaa likiwemo kabila la Gumuz. Hatahivyo katika miaka ya hivi karibuni wakulima na wafanyabiashara kutoka eneo jirani la Amhara wamehamia eneo hilo na kupelekea watu wa kabila la Gumuz kulalamika kuwa ardhi yao yenye rutuba imeghusubiwa.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya Abiy Ahmed, mkuu wa jeshi pamoja na maafisa wengine kutembelea eneo hilo na kutoa wito wa kuwepo utulivu baada ya kushtadi mapigano makali baina ya makabila mbali mbali katika miezi ya hivi karibuni. Mwezi uliopita watu 34 waliuawa baada ya basi kushambuliwa na genge la wabeba silaha.

Tags