Wanigeria waendeleza maandamano ya kutaka kuachiwa huru Sheikh Zakzaky
Wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) wamefanya maandamano makubwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka kuachiwa huru kiongozi wa harakati hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa jela kwa miaka kadhaa sasa.
Mjini Abuja, wafuasi wa IMN waliokuwa na mabango yenye maandishi na picha za Sheikh Zakzaky na mashahidi wa harakati hiyo walikuwa wakipiga nara zinazotaka kuachiwa huru mwanazuoni huyo wa Kiislamu na mkewe haraka iwezekanavyo.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake walikamatwa na vyombo vya dola vya Nigeria tarehe 13 Disemba mwaka 2015 katika shambulizi lililofanywa na askari wa nchi hiyo dhidi ya kituo cha kidini cha Baqiyyatullah katika mji wa Zaria.
Siku hiyo jeshi la Nigeria liliwafyatulia risasi Waislamu waliokuwa katika kituo hicho cha kidini na nyumba na msomi huyo na kuua shahidi mamia ya watu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky.
Katika miezi ya karibuni Wanigeria wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakitaka kuachiwa huru mwanazuoni huyo wa Kiislamu lakini jeshi na skari usalama wanakandamiza maandamano hayo.