Wanamgambo wa Ethiopia waishambulia Sudan; watu kadhaa wauawa
Raia kadhaa wameuawa na wengine hawajulikani walipo kufuatia shambulizi lililofanywa na wanamgambo wa Kiethiopia huko Sudan.
Wanamgambo wa Ethiopia wamelishambulia kijiji cha Leya eneo la El Fashaga El Sughra ndani ya ardhi ya Sudan na kuwauwa wanawake 5 na mtoto mmoja. Wanawake wengine wawili hawajulikani walipo kufuatia shambulio hilo la wanamgambo wa Ethiopia wanaojulikana kwka jina la Shifta.
Gazeti la Sudan Tribune limekinukuu chombo kimoja cha kuaminika na kuripoti kuwa, wanamgambo hao wa Ethiopia walitekeleza shambulio hilo jana adhuhuri wakati wakulima katika eneo la mpakani la Fashaga huko Sudan walipokuwa wakivuna mazao yao.
Jeshi la Sudan limeanza kuwasaka wanamgambo wa Ethiopia baada ya shambulio hilo. Gazeti la Sudan Tribune limeandika kuwa: Majeshi ya Sudan na Ethiopia yameimarisha uwepo wao katika maeno ya mipaka ya nchi mbili hizo ili kudhibiti harakati za wanamgambo wenye mfungamano na watu wa maeneo ya Tigray na Amhara nchini Ethiopia.