Jeshi la Ethiopia lamuua waziri wa zamani wa mambo ya nje
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65767-jeshi_la_ethiopia_lamuua_waziri_wa_zamani_wa_mambo_ya_nje
Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa , jeshi lake limemuua waziri wa zamani wa mambo ya nje Seyoum Mesfin, mmoja wa wanachama waanzilishi wa chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 14, 2021 10:00 UTC
  • Jeshi la Ethiopia lamuua waziri wa zamani wa mambo ya nje

Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa , jeshi lake limemuua waziri wa zamani wa mambo ya nje Seyoum Mesfin, mmoja wa wanachama waanzilishi wa chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF).

Taarifa zinasema Seyum aliuawa pamoja na wanachama wengine wa ngazi ya juu wa TPLF kaskazini mwa jimbo la Tigray, baada ya kukataa amri ya jeshi ya kujisalimisha.

Seyum  alihudumu kama waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia kutoka mwaka 1991 hadi 2010 na aliwahi pia kuwa balozi wa Ethiopia nchini China. Mwaka 2015 aliteuliwa kuwa mwakilishi wa jumuiya ya kieneo ya IGAD katika mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini.

Serikali ilikuwa imetoa waranti ya kukamatwa kwake pamoja na viongozi wengine wa ngazi ya juu katika TPLF – kufuatia oparesheni ya kijeshi ya mwezi Novemba eneo la Tigray.

Aidha imedokezwa kuwa, makumi ya wanachama wengine wa TPLF waliuawa na wengine kukamatwa katika oparesheni ya hivi punde.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliamuru oparesheni ya kijeshi dhidi ya jimbo la Tigray mnamo Novemba 4 na kuiondoa madarakani TPLF, baada ya vikosi vyake kuvamia kambi ya jeshi la kitaifa.

Serikali ya Addis Ababa, inaituhumu TPLF kuwa inataka kulitenganisha eneo la Tigray na ardhi ya Ethiopia. Hata baada ya Jeshi la Ethiopia kutangaza hivi karibuni kuwa limeudhibiti mji wa Mekelle, makao makuu ya eneo hilo,  lakini mapigano yanaripotiwa kuendelea.