Amnesty yasema Nigeria inajaribu kuficha mauaji ya raia mjini Lagos
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeituhumu serikali ya Nigeria kuwa inafanya jitihada za kuficha mauaji ya kutisha ya wananchi waliokuwa wakiandamana katika mji wa Lagos mwezi Oktoba mwaka uliopita.
Katika taarifa ya jana Alkhamisi, shirika hilo limesema Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi cha Polisi ya Nigeria (SARS) ndicho kinachopaswa kubebeshwa dhima ya kuua na kujeruhi idadi kubwa ya wananchi waliokuwa wakiandamana kwa amani Oktoba 20 mwaka uliopita 2020.
Osai Ojigho, Mkurugenzi wa Amnesty International nchini Nigeria amesema, "tangu ukatili huo wa maafisa usalama uliopelekea watu 12 kuuawa ufanyike, serikali ya Nigeria imekuwa ikiwaandama waungaji mkono wa maandamano hayo dhidi ya ukandamizaji uliokuwa ukifanywa na kikosi cha SARS."
Ripoti ya Amnesty International inaeleza kuwa, wanajeshi na askari polisi wa Nigeria waliwaua waandamanaji wasiopungua 12 katika maandamano hayo.

Askari wa jeshi la Nigeria waliripotiwa kuwafyatulia risasi waandamanaji hao katika mji wa Lagos na kisha kuiweka miili ya watu iliyowauwa ndani ya malori na kuipeleka kusikojulikana.
Maandamano hayo ya wananchi huko Nigeria yalianza tarehe 20 mwezi Oktoba mwaka jana, kulalamikia ukandamizaji wa polisi. Maandamano hayo yaliyofanyika kwa siku kadhaa mfululizo yalipelekea kuvunjiliwa mbali Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi (SARS).