Waziri Mkuu wa Kongo DR atangaza kujiuzulu na serikali yake
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sylvestre Ilunga Ilunkamba ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huo Ijumaa hii, siku moja baada ya Bunge la nchi hiyo kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Ilunga alimkabidhi Rais Felix Tshisekedi barua yake ya kujiuzulu Ijumaa ya jana, lakini Waziri Mkuu huyo na serikali yake wataendelea kuhudumu kwa muda hadi pale serikali nyingine itakapoteuliwa.
Wabunge walipasisha kwa kishindo hoja ya kumuengua madarakani Ilunga na serikali yake katika kikao cha Jumatano, wakimtuhumu kwa utepetevu. Hoja hiyo ilipasishwa kwa kura 367 kati ya 500 za Wabunge wa nchi hiyo.
Wabunge waliopasisha hoja hiyo wanasema serikali iliyobanduliwa ya muungano ilishindwa kutekeleza majukumu yake, na wanatumai serikali ijayo itashughulikia changamoto zinazolikabili taifa hilo kwa miaka miwili sasa.
Hatua hiyo ni ushindi kwa Rais Felix Tshisekedi ambaye mwezi Disemba mwaka uliopita, alitangaza kuvunja ushirikiano wa kuunda serikali na washirika wa karibu wa rais wa zamani Joseph Kabila.
Rais huyo amekuwa akipigania kufanikisha mpango huu ili kupata nguvu zaidi kutoka kwa washirika wake bungeni ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo, kinyume na namna mambo yamekuwa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.