Corona: Tanzania kuanza kampeni ya 'kupiga nyungu' wiki nzima
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa nchini Tanzania, Selemani Jafo ametangaza kuanza kampeni ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona juma lijalo.
Waziri Jafo amesema hayo akiwa katika ziara ya Rais wa Tanzania John Magufuli mkoani Tabora ambapo akizungumzia janga la virusi vya corona amesema, kuanzia kesho Jumatatu) kampeni ya kupambana na janga hilo itaanza.
''Hapa corona haina nafasi, tutaendelea kumuomba Mwenyezi Mungu, kama Mh.Rais ulivyotuelekeza na umesema watu wajifukize sana, na Rais naomba nikwambie Jumatatu (kesho) tunaanza kampeni nyingine ya juma zima season three (awamu ya tatu), nyungu kama kawaida, tunajifukiza, tunakula matunda, tunamuomba Mungu, tunaanza tarehe moja mpaka tarehe saba.
Siku ya Ijumaa, msemaji Mkuu wa serikali ya Tanzania Dkt. Hassan Abbas alisema, Tanzania inazingatia miongozo yote ya tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona na hata wakati huu ambao dunia inapambana na wimbi la pili la maambukizi ya virusi hivyo.
Hivi majuzi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli alitahadharisha kuhusu chanjo ya Covid 19 ambayo imeanza kutolewa katika mataifa mbalimbali duniani na kusisitiza pia kuwa, hategemei kutangaza hata siku moja ya kujifungia ndani, ingawa amesisitiza umuhimu wa kuchukua tahadharii na kumuomba Mungu.
Tanzania iliacha kutangaza takwimu za maambukizi au vifo vya virusi hivyo mwezi Aprili mwaka jana baada ya maafisa wa maabara ya taifa kutuhumiwa kutoa matokeo yasiyo sahihi. Aidha Rais John Pombe Magufuli alitangaza Julai mwaka jana (2020) kwamba, Tanzania haina tena virusi vya Corona baada ya siku tatu za maombi ya kitaifa.