Watu kadhaa wauawa katika shambulio la kigaidi la al-Shabaab Somalia
Kwa akali watu watatu wameuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa baada ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab kushambulia hoteli moja katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kwa mabomu na risasi.
Afisa wa polisi mjini Mogadishu, Ali Hassan ameliambia shirika la habari la DPA kuwa, zaidi ya watu tisa aghalabu yao wakiwa ni raia wameuawa katika hujuma hiyo ya jana Jumapili.
Inaarifiwa kuwa, wanachama wa al-Shabaab walivamia Hoteli ya Afrik iliyoko katika makutano ya barabara ya K-4 yenye shughuli nyingi, ambapo mripuko wa bomu ulisikika katika lango kuu la jengo lenye hoteli hiyo, kabla ya milio ya risasi kuhanikiza ndani ya mgahawa huo dakika chache baadaye.
Genge hilo la ukufurishaji lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda na ambalo limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya maafisa wa serikali na raia, limekiri kutekeleza hujuma hiyo ya jana.
Katika hatua nyingine, watoto wasiopungua wanane waliuawa jana Jumapili baada ya kuripukiwa na bomu katika eneo la Golweyn, kaskazini mwa mji wa pwani wa Merca, yapata kilomita 120 kusini mwa Mogadishu.
Aidha watoto wengine 11 wamejeruhiwa katika mkasa huo. Duru za habari zinaarifu kuwa, watoto walioaga dunia na kujeruhiwa kwenye tukio hilo la jana karibu na mji mkuu wa Somalia ni wa umri wa miaka 4 hadi 12.