Umoja wa Mataifa: Hali ya kibinadamu Tigray Ethiopia imezidi kuwa mbaya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i66640-umoja_wa_mataifa_hali_ya_kibinadamu_tigray_ethiopia_imezidi_kuwa_mbaya
Umoja wa Mataifa umetangaza tena kuwa, hali ya kibinadamu katika jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia imezidi kuwa mbaya na kwamba, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za haraka kushughulikia hali hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 08, 2021 22:59 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Hali ya kibinadamu Tigray Ethiopia imezidi kuwa mbaya

Umoja wa Mataifa umetangaza tena kuwa, hali ya kibinadamu katika jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia imezidi kuwa mbaya na kwamba, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za haraka kushughulikia hali hiyo.

Hayo yamo katika  ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa na gazeti la Democratic la Sudan inayoeleza kuwa, kuongezeka vurugu na machafuko katika jimbo hilo kumekwamisha kabisa upelekeaji wa misaada ya kibinadamu.

Sehemu nyingine ya ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, kungali kuna hatari kubwa ya kufanyika vitendo vya kihalifu na vilivyo dhidi ya binadamu katika eneo hilo.

"Endapo hakutachukuliwa hatua za maana na za haraka kwa ajili ya kuboresha hali ya kibinadamu katika jimbo la Tigray, hali hiyo itakuwa mbaya mno katika siku za usoni" imeeleza sehemu nyingine ya ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Wakimbizi Tigray

 

Ripoti hiyo imetolewa siku chache tu baada ya ripoti nyingine kama hiyo ya Umoja wa Mataifa ya Alkhamisi iliyopita ambayo ilieleza akthari ya wakazi wa eneo hilo linaloshuhudiwa mapigano hawana chakula, maji wala mahitaji mengine ya msingi.

Eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa Ethiopia lilishuhudia mapigano mwishoni mwa mwaka uliopita kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF.

Mbali na maelfu ya raia kuuawa, wengine karibu milioni moja wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.