Ethiopia yatoa idhini kwa wafanyakazi wa kibinadamu wa UN kufika Tigray
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i66664-ethiopia_yatoa_idhini_kwa_wafanyakazi_wa_kibinadamu_wa_un_kufika_tigray
Serikali ya Ethiopia imeyaruhusu mashirika ya Umoja wa Mataifa kuwatuma wafanyakazi zaidi wa misaada, katika mkoa uliokumbwa na machafuko wa Tigray.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 09, 2021 07:37 UTC
  • Ethiopia yatoa idhini kwa wafanyakazi wa kibinadamu wa UN kufika Tigray

Serikali ya Ethiopia imeyaruhusu mashirika ya Umoja wa Mataifa kuwatuma wafanyakazi zaidi wa misaada, katika mkoa uliokumbwa na machafuko wa Tigray.

Umoja wa Mataifa unasema eneo hilo linakabiliwa na tishio la njaa na kwamba sehemu kubwa ya mkoa huo imekuwa vigumu kufikiwa na wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya kiutu.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu kuelekea hakikisho kwamba wafanyakazi wa masuala ya kiutu mkoani Tigray wataweza kusambaza misaada inayohitajika.

Ripoti iliyotolewa wiki iliyopita ilisema kuwa maisha ya raia mkoani Tigray yamekuwa ya kutisha sana tangu mapigano yalipozuka mwezi Novemba baina ya vikosi vya serikali ya Ethiopia na vile vya mkoa wa Tigray.

Serikali inadai kwamba zaidi ya watu milioni moja katika mkoa huo wameweza kufikiwa na misaada, ingawa wafanyakazi wa mashirika ya kiutu wana ripoti tofauti.

Eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa Ethiopia lilishuhudia mapigano mwishoni mwa mwaka uliopita kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF.

Mbali na maelfu ya raia kuuawa, wengine karibu milioni moja wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.