Libya yawanusuru wahajiri 1,500 katika pwani ya nchi hiyo
Gadi ya Pwani ya Libya imefanikiwa kuwaokoa wahajiri haramu 1,500 waliokuwa hatarini kuzama katika maji ya pwani ya magharibi ya nchi hiyo katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
Adel al-Idrissi, afisa wa Kamati ya Kimataifa ya Uokozi amesema wahajiri hao wameokolewa katika operesheni kadhaa zilizofanywa na Gadi ya Pwani ya nchi hiyo ndani ya juma moja lililopita.
Naye Luteni Kanali Mohammed Abdel Aali wa Gadi ya Pwani ya Libya amesema jana Jumatano pekee wahamiaji haramu 240 wakiwa ndani ya boti mbili hafifu walinusuriwa katika operesheni iliyofanyika katika mji bandari wa Al-Khums, pwani ya magharibi mwa nchi.
Wapiga mbizi wa Gadi ya Pwani ya Libya wamesema wahajiri hao waliokolewa katika sehemu kadhaa za maji ya Bahari ya Mediterania wakiwa hatarini kuzama.

Libya ni moja ya vivuko muhimu zaidi vinavyotumiwa na wahajiri haramu wa Kiafrika, ambao kutokana na hali mbaya ya uchumi na usalama katika nchi zao au vita na ukame huamua kuhatarisha maisha yao kwa kuzihama nchi zao na kuelekea Ulaya kutafuta maisha bora kwa kutumia usafiri hatarishi wa baharini.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Uhamiaji Duniani (IOM), katika mwaka uliopita wa 2020, zaidi ya wahajiri haramu 1,200 walipoteza maisha katika Bahari ya Mediterania