RC: Makumi ya maelfu katika hatari ya kufa njaa Tigray, Ethiopia
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema sehemu kubwa ya eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa Ethiopia haifikiwi kabisa na misaada ya kibinadamu, na kwamba makumi ya maelfu ya wakazi wa eneo hilo wako katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na njaa.
Abera Tola, Rais wa Msalaba Mwekundu nchini Ethiopia amesema asilimia 80 ya eneo hilo halifikiki wakati huu ambapo mapigano yanaendelea kushuhudiwa.
Amesema shirika hilo linakadiria kuwa, watu milioni 3.8 katika eneo hilo lenye wakazi milioni 6 wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu, na kwamba makumi ya maelfu miongoni mwao wamebakia mifupa kwa kukosa lishe.
Hii ni licha ya serikali ya nchi hiyo kudai kwamba, zaidi ya watu milioni moja katika mkoa huo wameweza kufikiwa na misaada ya mashirika ya kibinadamu.
Eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa Ethiopia lilishuhudia mapigano mwishoni mwa mwaka uliopita kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF, na mapigano hayo yangali yanaendelea katika baadhi ya maeneo.
Mbali na maelfu ya raia kuuawa na kujeruhiwa, wengine karibu milioni moja wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.