Mchungaji wa Nigeria: Dhulma anazofanyiwa Sheikh Zakzaky ni dhulma dhidi ya ubinadamu
(last modified Mon, 15 Feb 2021 01:25:37 GMT )
Feb 15, 2021 01:25 UTC
  • Mchungaji wa Nigeria: Dhulma anazofanyiwa Sheikh Zakzaky ni dhulma dhidi ya ubinadamu

Mchungaji mmoja wa Nigeria amewataka wananchi wote wa nchi hiyo kufanya jitihada za kuhakikisha Sheikh Ibrahim Zakzaky anaachiwa huruu na anaamini kuwa, dhulma inayofanywa dhidi ya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni dhulma dhidi ya wanadamu wote.

Mchungaji John Joseph ambaye ni miongoni mwa wachungaji mashuhuri nchini Nigeria amesema kuwa, zimefanyika jitihada za kuhakikisha Sheikh Zakzaky anaachiwa huru na juhudi hizo bado zinaendelea. Ameongeza kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky ni mwakilishi wa amani na utulivu katika jamii ya Nigeria na amekuwa akitetea haki za binadamu wote, hakutofautisha baina ya wananchi wa dini tofauti wala baina ya Waislamu na Wakristo.

Mchungaji huyo mashuhuri wa Nigeria amesema: "Ushirikiano wa serikali ya Nigeria na utawala wa Kizayuni wa Israel umeibua wasiwasi na kwa msingi huo tunaamini kwamba, kila upande unaohusika katika kadhia hii ni adui wa ubinadamu."

Hivi karibuni Prf. Umar Zaky ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu nchini Nigeria alisema kuwa, serikali ya Abuja inashirikiana na Saudi Arabia katika kukandamiza Waislamu wa madhehebu ya Shia na pande hizo mbili zinaogopa hata kuona habari zinazohusiana na Sheikh Zakzaky zikitangazwa kwenye vyombo vya habari.

Sheikh Zakzaky

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walikamatwa na vyombo vya usalama vya Nigeria tarehe 13 Disemba mwaka 2015 wakati wa shambulizi la jeshi la nchi hiyo dhidi ya kituo cha kidini za Baqiyatullah kwenye mji wa Zaria. 

Mamia ya Waislamu wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky waliuawa shahidi katika shambnulizi hilo.