Maporomoko ya ardhi yasababisha vifo vya watu 20 Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6688-maporomoko_ya_ardhi_yasababisha_vifo_vya_watu_20_rwanda
Kwa akali watu 20 wameaga dunia na wengine kadhaa kuachwa bila makazi kufuatia maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini Rwanda.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2016 23:10 UTC
  • Maporomoko ya ardhi yasababisha vifo vya watu 20 Rwanda

Kwa akali watu 20 wameaga dunia na wengine kadhaa kuachwa bila makazi kufuatia maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini Rwanda.

Frederic Ntawukuriryayo, Msemaji wa Wizara Inayoshughulikia Majanga wa Rwanda ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, akthari ya waliouawa katika maporomoko hayo ya usiku wa kuamkia jana Jumapili katika wilaya ya Gakenke, kaskazini mwa nchi ni watoto wadogo.

Ntawukuriryayo amesema serikali imewaondoa watu waliokuwa katika maeneo hatari na kuwapeleka maeneo salama ili kuepuka maafa zaidi. Amesema mvua zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo ya Rwanda zimesababishwa na taathira za mabadiliko ya hali ya hewa yanayotokana na El Nino.

Zaidi ya watu 67 wameuawa katika maeneo mbali mbali ya Rwanda kutokana na taathira za janga hilo la kimaumbile tokea Januari hadi Aprili mwaka huu, huku 12 kati yao wakiuawa katika tukio moja viungani mwa mji mkuu Kigali, ambapo nyumba zaidi ya 1500 ima zilibomolewa na maporomoko ya ardhi au kusombwa na mafuriko.

Makumi ya watu wamepoteza maisha na maelfu ya wengine wamebaki bila makazi kutokana na mvua hizo zinazoendelea kunyesha katika nchi za kanda ya Afrika Mashariki na haswa Kenya na Tanzania.