Jeshi la DRC laua wanamgambo 16 kaskazini mwa nchi
(last modified 2021-03-02T03:15:24+00:00 )
Mar 02, 2021 03:15 UTC
  • Jeshi la DRC laua wanamgambo 16 kaskazini mwa nchi

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza habari ya kuua wanamgambo 16 katika makabiliano makali baina ya pande mbili hizo huko kaskazini mashariki mwa nchi.

Luteni Jules Ngongo, msemaji wa jeshi katika mkoa wa Ituri kaskazini mwa DRC alisema hayo jana Jumatatu na kuongeza kuwa, wanamgambo hao wameuawa katika operesheni ya wanajeshi wa nchi hiyo iliyoanza tokea Ijumaa.

Kadhalika wanachama wengine saba wa kundi la wanamgambo la Patriotic and Integrationist Congo Forces (FPIC) wametiwa mbaroni katika operesheni hiyo.

Luteni Ngongo ameeleza bayana kuwa, wanajeshi watatu wa Kongo DR wameuawa katika makabiliano hayo ya siku tatu.

Moja ya magenge ya waasi nchini DRC

Hii ni katika hali ambayo, juzi Jumapili, watu wenye silaha wanaodhaniwa ni waasi wa ADF waliripotiwa kuua watu 10 katika mashambulizi tofauti huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Waasi wa ADF wana asili ya Uganda na wameweka kambi zao katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwaka 1995.

 

Tags