Wafuasi wa Sheikh Zakzaky wawaadhimisha mashahidi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria
Wafuasi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria (IMN) wamefanya hafla ya kuwaenzi mashahidi wa harakati hiyo.
Wafuasi wa kiongozi wa harakati hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky, jana walifanya hafla maalum ya kuwakumbuka na kuwaenzi mashahidi wa harakati hiyo katika Siku ya Mashahidi iliyosadifiana na kumbukumbu ya siku aliyokufa shahidi Imam Mussa al Kadhim (as). Hafla hiyo ilifanyika kando kando ya mji mkuu wa Nigeria, Abuja.
Katika hafla hiyo, wafuasi wa harakati ya Kiislamu nchini Nigeria walibeba pia picha za mashahidi hao wa harakati hiyo.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe wangali wanashikiliwa kwenye jela za serikali ya Nigeria tangu walipotiwa nguvuni Desemba 13, 2015 wakati askari wa jeshi la serikali walipovamia na kushambulia Husainiya na nyumba ya kiongozi huyo wa kidini katika mji wa Zaria jimboni Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo, ambapo waliwaua shahidi mamia ya Waislamu wakiwemo wana watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky.
Licha ya amri rasmi iliyotolewa na mahakama, serikali ya Nigeria hadi sasa imekataa kumwachia huru Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe kwa visingizio tofauti na hata imemzuilia kupatiwa huduma za matibabu licha ya hali yake ya afya kuripotiwa kuwa mbaya.
Katika miezi ya karibuni, wananchi wa Nigeria wamefanya maandamano ya amani mara kadhaa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kutaka Sheikh Zakzaky aachiwe huru, lakini kila mara vikosi vya usalama vimetumia mkono wa chuma kuzima maandamano hayo.../