Makumi wapoteza maisha kwenye mkasa wa moto kiwandani Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i67780-makumi_wapoteza_maisha_kwenye_mkasa_wa_moto_kiwandani_misri
Makumi ya watu wamefariki dunia huku wengine wengi wakijeruhiwa kutokana na ajali ya moto iliyokikumba kiwanda kimoja cha nguo katika mji mkuu wa Misri, Cairo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 12, 2021 02:42 UTC
  • Makumi wapoteza maisha kwenye mkasa wa moto kiwandani Misri

Makumi ya watu wamefariki dunia huku wengine wengi wakijeruhiwa kutokana na ajali ya moto iliyokikumba kiwanda kimoja cha nguo katika mji mkuu wa Misri, Cairo.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Misri imesema, mkasa huo ulitokea jana Alkhamisi katika kiwanda cha nguo kilichoko katika wilaya ya Obour, viungani mwa mji mkuu Cairo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mbali na watu 20 kupoteza maisha katika ajali hiyo ya jana, wengine zaidi ya 24 wamejeruhiwa na wanatibiwa katika hospitali na zahanati za eneo hilo.

Wazima moto wakiwa kazini

Serikali ya Cairo bila kutoa maelezo zaidi imesema timu ya wataalamu imeanzisha uchunguzi wa kubaini kiini cha moto huo na athari zake katika majengo yanayopakana na kiwanda hicho kilichoko katika jengo lenye orofa nne.

Duru za hospitali zinaarifu kuwa, yumkini idadi ya vifo ikaongezeka kutokana na majereha mabaya waliyoyapata manusura wa mkasa huo wa jana Alkhamisi.