Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania afariki dunia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amefariki dunia katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu.
Taarifa za kifo cha Rais Magufuli, zilitangazwa jana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye amesema Magufuli alifariki dunia saa 12 jioni kwa maradhi ya moyo baada ya kulazwa katika hospitali hiyo tangu Machi 6.
Amesema awali, Rais Magufuli alifikishwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Machi 6 akisumbuliwa na tatizo la moyo la mfumo wa umeme ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10.
Mama Samia amesema, “Machi 14 mwaka huu, alijisikia vibaya akakimbizwa hospitali ya Mzena ambako aliendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hadi umauti ulipomkuta."
Aidha Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema nchi itakuwa katika maambolezo kwa muda wa siku 14 na bendera zitapepea nusu mlingoti. Ameongeza kuwa, wananchi watajulishwa juu ya taratibu za mazishi za kiongozi huyo mkuu wa nchi.
Magufuli alionekana mwisho hadharani Februari 27, wakati akimuapisha Dk Bashiru Ally baada ya kumteua kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Tanzania kuchukua nafasi ya Balozi John Kijazi aliyefariki dunia Februari 17, 2021.
Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, baada ya Rais wa Magufuli kufariki dunia, hakuna uchaguzi mwingine unaofanyika katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na badala yake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ataapishwa kuwa Rais kwa kipindi kilichosalia katika muhula wa miaka mitano.