Tanzania yabadilisha tarehe ya kumzika Magufuli, hayati ameagwa leo Dar es Salaam
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i68110-tanzania_yabadilisha_tarehe_ya_kumzika_magufuli_hayati_ameagwa_leo_dar_es_salaam
Ibada ya wafu ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli imefanyika leo katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
(last modified 2025-11-05T05:46:17+00:00 )
Mar 20, 2021 12:18 UTC
  • Tanzania yabadilisha tarehe ya kumzika Magufuli, hayati ameagwa leo Dar es Salaam

Ibada ya wafu ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli imefanyika leo katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii pamoja na wananchi wa matabaka mbalimbali wamehudhuria ibada hiyo, ambapo wamemtaja hayati Magufuli kama kiongozi mzalendo aliyetanguliza mbele maslahi ya wananchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mama Maria Nyerere, mjane wa aliyekuwa rais mwanzilishi wa taifa la Tanzania  Julius Kambarage Nyerere ni miongoni mwa shakhsia mashuhuri waliojitokeza kuuaga mwili wa mwendazake katika uwanja wa Uhuru hii leo.

Huku hayo yakiarifiwa, ratiba ya mazishi ya hayati Magufuli imebadilishwa na sasa atazikwa Machi 26 badala ya Machi 25 iliyopangwa hapo awali.

Kesho Jumapili  Machi 21, wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo jirani watapata fursa ya kuuaga mwili huo na kisha utasafirishwa kwenda Dodoma ambapo wananchi wa mkoa huo watatoa heshima zao za mwisho Jumatatu Machi 22.

Mjane wa Dkt Magufuli akitoka kuuaga mwili wa mwendazake

Wananchi wa Zanzibar nao watapata fursa ya kuuaga Jumanne Machi 23 kisha utasafirishwa kuelekea Mwanza na utaagwa Jumatano Machi 24. Alkhamisi Machi 25 wanafamilia na wananchi wa Chato mkoani Geita na mikoa ya jirani wataungana kwa pamoja kuuaga mwili wa kiongozi huyo kabla ya kuzikwa kesho yake Machi 26.

Hapo jana, Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kufuatia kifo cha Magufuli kilichotokea siku ya Jumatano kutokana na kile kilichotajwa kuwa matatizo ya moyo.